Tuesday, July 26, 2011

Kikao cha FAO chaanza rasmi mahsusi kwa eneo la Pembe ya Afrika

Ukame uliokithiri: Mifugo yafa kwa wingi na njaa imesambaa Ethiopia 

Ukame mbaya umelikumba eneo la Pembe ya Afrika na kusababisha tishio kubwa la njaa pia nchini Ethiopia. Wakati huo huo juhudi za kuyaokoa maisha ya mamilioni ya watu zitaimarishwa kwenye kikao cha FAO. 


Wajumbe wa serikali, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na wa mashirika ya misaada leo wanakutana mjini Rome kwa ajili ya kikao cha dharura kulijadili baa la njaa kwenye eneo la Pembe ya Afrika. Wajumbe kwenye kikao hicho wanazungumzia njia za kuwasaidia watu wapatao milioni 12 waliomo katika hatari ya kufa njaa.

Kikao hicho kinafanyika kufuatia shinikizo la kimataifa kuwataka viongozi wa dunia waongeze misaada kwa ajili ya mamilioni ya watu wanaotishiwa na baa la njaa lilisosababishwa na ukame mbaya ambao haujawahi kuonekana katika historia ya miaka 60 iliyopita katika eneo la Pembe ya Afrika. 

Marekani na Israel zalaumiwa kwa kukwamisha umoja wa kitaifa Palestina


Kiongozi mmoja wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina ameilaumu Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kukwamisha ufanikishaji wa vipengee vya makubaliano ya umoja wa kitaifa Palestina.

Abu Ali Shakib, mmoja wa viongozi waandamizi wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amesema kuwa, mchakato wa kuelekea kwenye umoja wa kitaifa ulioingia kasi kubwa baada ya kufikiwa makubaliano kati ya HAMAS na Fat'h umewatia hofu mabeberu wa dunia wakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni kiasi kwamba Rais Barack Obama wa Marekani amekuwa akiingilia waziwazi mapatano hayo kupitia kumshinikiza Mahmoud Abbas na serikali yake kujiweka mbali na HAMAS.

Huku hayo yakiripotiwa, Salam Fayyadh, Waziri Mkuu wa serikali ya Mahmoud Abbas amesema kuwa, yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ili kurahisisha utekelezaji wa makubalino ya umoja wa kitaifa ya Palestina.

Fayyadh amesema hayo alipohojiwa na televisheni ya serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Matamshi hayo ya Salam Fayyadh yamekuja baada ya kuongezeka mashinikizo na lawama dhidi yake kutokana na kukubali kuburuzwa na madola ya kigeni ikiwemo Marekani.